Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
MKUU wa wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle ametoa agizo kwa watu ambao bado wanaoishi kwenye maeneo yaliyozingirwa na maji ,mabondeni waondoke na kuhamia kwenye maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya usalama wao.
Akipokea misaada mbalimbali yenye thamani ya milioni 28 kutoka Taasisi ya WHO IS HUSSAIN, kwa ajili ya waathirika wa mafuriko Rufiji, Gowelle alisema, Serikali inaendelea kutoa maeneo ya kutosha ili kuhakikisha wapo salama.
Alieleza ,kijiji cha Chumbi kimetoa eneo, kwasasa wanaendelea kulipima litakuwa na viwanja 500 kwa ajili ya makazi yaliyo salama.
Aidha Gowelle alieleza, wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) imetoa eneo Muhoro, na Serikali kutoa kwa wananchi ambapo vimetengwa viwanja 600 .
Alieleza, kazi kubwa inaendelea kufanyika kwani mvua bado zinaendelea kunyesha.
Vilevile alifafanua kwamba, katika kambi ya Chumbi kulikuwa na waathirika wa mafuriko 498 sasa wamebakia 311 ,kaya zilikuwa 117 kwasasa zimebakia 82.
"Watu wote 89,000 wengine wapo kwa ndugu, jamaa na marafiki,nao hao tunaendelea kuwawezesha kwasababu kwa hali ya kawaida kama mtu ukipokea kaya 3 zenye watu 11 alikuwa anakula debe mbili, hivyo kwasasa atahitaji debe 10 ,kwahiyo misaada hii tunayopokea tunashukuru Sana wadau hawa" alisema Gowelle.
Alisema, mafanikio hayo yametokana na mh Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha uwezo wake mkubwa katika kujenga mahusiano na Taasisi ndani na nje .
Gowelle alimpongeza Rais Samia kwa kutoa tani 300 za chakula, kupeleka vifaa tiba,madawa kupitia MSD kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohammed Mchengerwa kwa jitihada zake za kutafuta wadau,ambapo hadi sasa imefikia milioni 107.7 fedha ambayo wataenda kununulia mbegu ,mchakato umeanza ili baadae waathirika wanaojishughulisha na kilimo warejee kwenye kilimo na yeye amechangia milioni 50.
Akizungumza baada ya kukabidhi misaada kambi ya Chumbi, mratibu wa mradi wa Taasisi ya WHO IS HUSSAIN ,Mohsin Bharwani alisema ,WHO IS HUSSAIN inajishughulisha na kusaidia jamii katika mambo mbalimbali ikiwemo kujenga visima, shule.
"Wakati changamoto ya mafuriko inaanza tulimuona kwenye vyombo vya habari Mbunge wa jimbo Mchengerwa akitoa misaada na kuomba wadau kushirikiana na Serikali kuchangia waathirika "alisema Mohsin.
Mohsin alisema, wameguswa na kuanza kuchangishana na washirika wao wengine na kufanikiwa kupata misaada hiyo.
Kwa upande wake Fatema Kermali kutoka WHO IS HUSSAIN alisema,wametoa mchele kilo 2,000, magodoro 110, maharage 900,sukari 1,400 ,sembe 1,500,mafuta lita 1,200,pedi, miswaki na sabuni vyote vina thamani ya Mil.28.
Kwa mujibu wa tathmini ,Wilaya ya Rufiji ni moja ya wilaya nchini iliyokumbwa na changamoto ya mafuriko kwa kiasi kikubwa,na kuathiri kata 12 kati ya 13 zilizopo, kusababisha vifo 8 , waathirika 89,000, kaya 23,360,makazi,Nyumba 628.
Serikali imetenga kiasi cha TZS bilioni 18.5 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini zitakazotolewa kama mikopo yenye masharti nafuu kupitia Benki ya NMB.
Makubaliano ya utaratibu wa ufadhili huo yalitiwa saini leo jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Bi Ruth Zaipuna, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe kwa niaba ya Serikali na kushuhudiwa na mkuu wa wizara hiyo, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima.
Akizungumza kabla ya utiaji saini ya mkataba huo wa miaka miwili, waziri huyo alisema wafanyabiashara wadogo na wa kati watakopeshwa fedha hizo kwa riba ya asilimia saba.
“TZS bilioni 18.5 ni hela nyingi za kuanzia lakini kiasi hiki kitaongezeka kwani lengo la Serikali ni kuifanya mikopo hii kuwa endelevu ili iwafikide watu wengi,” Dkt Gwajima alibainisha huku akisisitiza umuhimu wa kuitumia vizuri na kuirejesha kwa wakati.
Aliongeza kuwa fedha hizo zikiwekezwa vizuri zinaweza kuwa na tija kubwa kimaendeleo kwa kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha mapato ya kaya.
Dr Gwajima alisema mikopo hiyo ni sehemu ya utaratibu mpya wa Serikali kuyawezesha makundi maalum na kuhakikisha wanufaika wake ni wale tu waliolengwa kupata usaidizi huo.
“Wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kwa hiyo Serkali kupitia wizara hii ina kila sababu ya kuwakwamua na kuwawezesha ikiwemo kupitia mikopo hii nafuu ambayo NMB imeanza kuitoa leo.”
Kwa mujibu wa Dkt Shekalaghe utiaji saini na NMB kukopesha fedha hizo kumeitimisha mchakato wa wizara yao kuitafuta benki mshirika katika masuala mbalimbali ya kiutendaji na kimaendeleo.
Akibainisha kuwa mafungu ya mikopo hiyo nafuu itatoka kila mwaka, katibu mkuu huyo alisema Serikali imeanzisha utaratibu mpya wa kuyafadhili makundi maalumu na tayari uandikishaji ya wale wenye sifa stahiki umeanza na kwa upande wa wajasiriamali pia wanapewa vitambulisho maalum.
Katika maelezo yake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna alisema mkataba wa kutoa mikopo hiyo ni kielelezo cha jitihada kubwa zinazofanywa na benki hiyo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wote nchini wakiwemo wale wadogo.
Aidha, alisema benki hiyo ina uzoefu na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wajasiriamali ambao umeifanya kutambulika kimataifa kama kinara wa kuzifadhili biashara changa, ndogo na za kati nchini.
“Tuzo tulizozipata mwaka huu katika hilo ni pamoja na zile za Benki Bora ya Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati na Benki Bora ya Uwezeshaji wa Biashara Ndogo na za Kati,” Bi Zaipuna alisema.
“Ukweli huo unadhihirishwa na idadi ya mikopo 129,540 yenye thamani ya TZS trilioni 2.03 iliyotolewa na NMB kwa wajasiriamali kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2023,” aliongeza na kueleza kuwa ukopeshaji huo kwa wajasiriamali wakiwemo wamachinga na boda boda ulikuwa ni wastani wa mikopo 2,699 kila mwezi na TZS bilioni 42.3 kwa mwezi.
“Historia ya Benki ya NMB imejengwa kupitia uwezeshaji wa sekta ya biashara ndogo na za kati, kutoa mikopo na juhudi za kuwafikia wafanyabiashara ni moja ya vipaumbele katika mpango mkakati wetu,” alifafanua.
Bi Zaipuna alimwambia Dkt Gwajima kuwa utiaji saini mkataba kati ya NMB na wizara yake kutapanua wigo wa kuwafikia wafanyabiashara wengi zaidi wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo nchini.
Pia alisema taasisi hiyo inajivunia kushirikishwa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika utekelezaji wa mipango ya kuwahudumia wajasiriamali kwa lengo la kukuza biashara zao na kuwapa fursa ya kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na pato la taifa kwa ujumla.
Akisisitiza umuhimu wa wajasiriamali katika maendeleo, Bi Zaipuna alisema shughuli zao ni zaidi ya asilimia 95 ya biashara zote rasmi duniani zikichangia asilimia 50 ya pato la taifa kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na zaidi ya asilimia 80 ya ajira zote barani Afrika.
“Pamoja na utoaji mikopo tunaamini kuwa wafanyabiashara hawa watafaidika pia na huduma nyingine mbalimbali za kifedha zinazotolewa na benki yetu na hivyo kuwafanya wakue kibiashara,” alibainisha huku akitilia mkazo umuhimu wa kuwapa elimu ya fedha ili kuhakikisha wanakuwa na nidhamu nzuri ya matumizi ya mikopo hiyo.
RC Chongolo ameeleza kuwa changamoto ya uharibifu mkubwa wa miundombinu umefanyiwa kazi kwa haraka na timu ya wataalamu wa TANROADS na TARURA jambo ambalo limerejesha mawasiliano ya pande zote zilizokuwa hazipitiki.
"Kila mmoja kwa barabara zake wamefanya kazi kubwa na wanaendelea kufanya hivyo lengo ni kuhakikisha Wananchi hawakosi huduma ya barabara pale inapotokea changamoto’’ Amekaririwa Mhe Chongolo.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe Mhandisi Suleiman Bishanga akizungumza mara baada ya kukagua sehemu zilizoathirika na mvua za El-Nino wilayani Songwe na Ileje amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 5.7 kwa ajili ya kutatua changamoto na kurejesha miundombinu ya barabara na madaraja ambayo yameharibiwa na mvua kubwa za El- nino zinazoendelea kunyesha Mkoani Songwe.
Amesema kuwa Wilayani Songwe miundombinu imeharibika katika barabara ya Galula – Namkukwe sehemu ya Malangali, daraja la Mpona maji yalifurika juu na kukata mawasiliano kati Kijiji cha Namkukwe na Mpona.
Sehemu nyingine ni Magamba eneo linalounganisha Kijiji cha Mpona na Igalula ambako sasa hivi linajengwa daraja na kuinua tuta la barabara; pia kwenye barabara ya Chang’ombe - Mkwajuni eneo la Zira miaka ya nyuma lilikuwa korofi; lakini mwaka huu halijapata changamoto kwa sababu Serikali kupitia TANROADS ilichukua hatua za mapema kulifanyia matengenezo.
Ameeleza kuwa Wilayani Mbozi Barabara iliyoathirika zaidi ni Mlowo – Kamsamba ambayo inaunganisha Mji wa Songwe kuelekea upande wa Mkoa wa Rukwa ambapo Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni moja kutengeneza maeneo mbalimbali yaliyoharibika.
“Katika Wilaya ya Momba kuna barabara ambayo tumeirithi mwaka jana kutoka TARURA kuja TANROADS na yenyewe ilikuwa katika hali mbaya, Serikali haikusita ikatupa fedha shilingi milioni 500 ambazo zimeenda kushughulikia matatizo ya kule na sasa ile Barabara ya Kwenda Ilonga inapitika’’ ameeleza Mhandisi Bishanga na kuogeza.
“Wilaya ya Mbozi kuelekea Ileje kuna sehemu tunaunganishwa na Daraja la Hezya lile dadaja lilisombwa na maji na Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 261 kwa ajili ya kujenga daraja hilo na kwa sasa linapitika’’.
Kwa upande wao Afisa Tarafa ya Songwe Godwin Kaunda na Diwani kata ya Magamba Mhe Kapala Chakupewa Makelele wameishukuru serikali kupitia TANROADS kwa urejeshaji wa haraka kwa miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathiriwa na mvua za El-Nino zinaendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini.